Yafuatayo ni majibu ya Zitto Kabwe kuhusu baadhi ya maswali yaliyoulizwa katika makala ya 'Waandishi Wanawalinda Wanasiasa Wanaokopa Wananchi?' iliyochapishwa katika blogu ya Udadisi:
Naomba kujibu baadhi ya mambo
Kuna matamko tofauti unayoyachanganya. Kuna Tamko la wakati wa uzinduzi wa Chama mwezi March mwaka 2015. Hili halikuwa la kutekeleza sheria ya maadili ya viongozi bali kutekeleza masharti ya katiba ya Chama. Maelezo yote mule yalitokana na kipindi cha ubunge wa 2010-2015. Madeni yote mule yanaisha kulingana na Ubunge. Kwa nini? Kwa sababu mikopo ile hulipwa kutokana na kipato cha ubunge na guaranteed na Bunge. Hivyo kila mwezi mbunge hukatwa kulipia deni mpaka muda wa ubunge unapoisha na mkopo huisha. Ni mikopo inayoitwa personal loans.
Mwaka 2010-2015 sikukopa NSSF bali nilikopa NMB. Deni lile lilikwisha pamoja na lile la CRDB.
Madeni unayoona sasa ni madeni ya mwaka 2016 na hizo unazoona ni balance baada ya malipo. Kila mwezi kutoka kwenye mshahara unakatwa kulipia deni na linakuwa limekwisha baada ya miezi 60 (miaka 5).
Mimi ni Mwanachama wa NSSF tangu mwaka 2004 nikiwa mtumishi wa FES. Naweka akiba NSSF kila mwezi kwa miaka 12 sasa. Mimi pamoja na wabunge wengine tunakopa NSSF kwa Sababu 1) kuna fao hilo la mikopo kwa wanachama kwa guarantee ya mwajiri 2) riba yake ni nafuu na 3) ni mkopo salama maana unakatwa moja kwa moja kutoka kwenye kipato cha kila mwezi.
Pia mwaka 2016 nimetambua madeni niliyorithi kutoka kwenye Chama kwa sababu chama hakina uwezo kulipa. Mikopo mingi niliyochukua ilikuwa ni kulipa madeni ya uchaguzi na nikabakiwa na madeni 2.
Kuhusu Gombe Advisors na Leka Dutigite hakuna mabadiliko yeyote ndio maana huandiki tena upya. Kimsingi mwaka huu ilitakiwa kisheria kuandika ongezeko na pungufu la mali na madeni tu. Haikutakiwa kuandika upya. Kwenye maelezo ya ziada nimeeleza sababu za kuandika upya. Nyaraka za maslahi ya zamani zinakuwa Tume ya Maadili kwenye file langu. Hivyo ukitaka kuelewa tamko la sasa ni lazima usome na tamko la mwaka uliopita kama ulivyofanya. Narudia, hatupaswi kurudia tamko kila mwaka bali unaweka tofauti zilizotokea.
Nashukuru kwa kuendeleza mijadala hii. Nguvu hii itumie kuwataka viongozi wengine wa umma kuweka matamko yao wazi hasa Rais na Mawaziri. Blogu yako itakuwa imesaidia sana umma. Natumai utaweza kurekebisha andiko lako kwa kuzingatia taarifa hizi ambazo hukuwa nazo. Naamini nitakuwa nimejibu baadhi ya maswali yako na kauli za kihusuda za Rais Magufuli kuhusu wanasiasa kukopa kana kwamba ni dhambi ama yeye hakuwa anakopa alipokuwa mbunge kwenye taasisi hizi.