Quantcast
Channel: UDADISI
Viewing all articles
Browse latest Browse all 468

Waandishi Wanawalinda Wanasiasa Wanaokopa?

$
0
0
Waandishi Wanawalinda Wanasiasa Wanaokopa Wananchi?
  
Chambi Chachage


Matukio matano yamenichochea kuandika makala haya. Kwanza, ni harakati za kulinda ‘Uhuru wa Kujieleza’. Pili, semina ya Kavazi la Nyerere iliyotolewa na Profesa Carlos Nuno Castel-Brancokuhusu‘Deni la Taifa’. Tatu, taarifa ya gazeti la Tanzania Daima kuhusu uwezekano wa chama cha ACT Wazalendo kufilisiwa. Nne, tangazo la Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe, kuhusu madeni yake. Tano, mahojiano ya Rais John Magufuli na wahariri yaliyogusia madeni ya wanasiasa.

Kwa wachambuzi wa tasnia ya habari, halikuwa jambo la kushangaza kuona Tanzania Daima ikichapisha katika ukurasa wake wa mbele kwamba ‘Zitto, ACT-Wazalendo Hatarini Kufilisiwa.’ Gazeti hilo linajulikana kama ‘kinywa’ cha chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho kilimvua uwanachama Zitto. Hivyo, siyo jambo la ajabu kuona likipata ujasiri wa kujaribu kuanika habari za Naibu Katibu Mkuu huyo wa zamani wa chama hicho. Ndiyo maana mwana-ACT, Dotto Rangimoto, amehoji kwenye Jamii Forums kama ‘Mbowe anasaka "Kiki" kwa jina la Zitto?’

Siku hiyo hiyo ya tarehe 27 Desemba 2016, Zitto alitoa tamko lililosajiliwa na "Wakili na Kamishna wa Viapo", Emmanuel Mvula. Tamko hilo lililowekwa katika vyanzo mbalimbali mtandaoni tarehe 30 Desemba 2016 linatoa ufafanuzi kuhusu deni ambalo gazeti la Tanzania Daima lilikuwa linajaribu kulianika na kulijengea hoja kwa kutumia taarifa ya madai ya madeni inayomhusisha mdai Soraya Souleymane. Hilo nalo halishangazi kwani baada ya kuwasisitizia watimize ahadi yao ya kutoa taarifa za gharama za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ACT-Wazalendo walizitoa mtandaoni tarehe 15-16 Februari 2016 ambapo jina la mdai huyona wengineo yaliwekwa wazi.

Hivyo, kitu kilichotuacha na butwaa baadhi yetu ni taarifa hii katika tamko hilo la mwaka huu: “NINA DENI LA TZS 191,060,094. HILI DENI LINATOKANA NA MKOPO KUTOKA NSSF.” Kwa nini linashangaza? Mosi, ni kwa sababu tamko hilo halituambii ni lini fedha hizo zilikopwa. Pili, ni kwa sababu katika tamko lake la aina hiyo la tarehe 29 Machi 2015 deni hilo halikuorodheshwa. Tatu, kutokuwepo kwa taarifa hizo kunatufanya tusijue kama zilikopwa wakati Zitto alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo ‘inaisimamia’ NSSF.

Utata huo umepelekea wadadisi wa mambo tuikumbuke hoja hii ya Rais Magufuli wakati wa mahojiano na wahariri wa vyombo vya habari tarehe 4 Novemba 2016:


Wadau wa 'hashtag' ya #UhuruWaKujieleza tunapaswa kuifanyia kazi changamoto hiyo. Bila ajizi Rais amesisitiza kwamba waandishi tunawalinda wanasiasa waliokopa katika taasisi zetu za umma. Bahati nzuri mwanasiasa mmojawapo amekuwa muwazi kwa kiasi chake kuhusu madeni yake ya NSSF na haya mengine: “NINA DENI LA TZ 176,315,106.21. HILI NI DENI LINALOTOKANA NA MKOPO KATIKA BANK YA CRDB.” Je, tutegemee tu utashi na uadilifu wa wanasiasa au turasimishe uwazi na uwajibikaji wao?

Changamoto iliyobaki kwetu ni kuwabana wanasiasa wengine nao wawe wakweli na wawazi au, kama alivyosema Rais, waandishi tuwachambue na kuwaanika hadharani bila kupepesa macho. Pia kwa ambao wamejitahidi kuwa wawazi tusiishie kuwapongeza tu. Tunatakiwa pia kuweka mapenzi na ushabiki wetu kwao pembeni na kuwauliza maswali magumu kuhusu namna walivyopata mikopo na jinsi ambavyo watalipa madeni ili Watanzania wote tufaidike.
Zitto ameonesha mfano. Kaonesha na ujasiri wa kujibu maswali yaliyoibuka kuhusu tamko lake ambapo amesisitiza kuwa anaamini “kwamba uwazi ni moja ya silaha madhubuti ya kupambana na ufisadi”. Hivyo, kawasilisha “muswada bungeni kutaka uwazi huu liwe sharti la sheria za nchi yetu.” Kupitia tamko lake rasmi pia:


 Sasa ni jukumu la waandishi kumuuliza Zitto naye atoe ufafanuzi kuhusu baadhi ya zinazoonekana kama tofauti kati ya taarifa yake ya mwaka jana na ya mwaka huu. Kwa mfano, taarifa ya mwaka huu haionekani ikiyataja makampuni ya Gombe Advisors Limited na Kigoma Development Initiatives (KDI) Limited ambayo mwaka jana aliyaorodhesha. Je, ameacha kumiliki hisa katika makampuni hayo ambayo amekuwa anasisitiza kwamba siyo ya kupata faida? Kama na yenyewe yalikopa, je, madeni hayo yameshalipwa? Na kama umiliki wake umebadilika, nani ni mmiliki wake? Maswali kama haya ni muhimu hasa ukizingatia kwamba tarehe 10 Desemba 2016 aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Leka Dutigite ambayo ilikuwa ina uhusiano wa kihisa na GombeAdvisors, Habib Mchange, alitoa taarifa kwa umma kuhusu ‘KUJIVUA UANACHAMA WA ACT WAZALENDO NA KUTOSHIRIKI SIASA’ ili apate “muda mwingi zaidi kufanya na kusimamia shughuli” zake “za kijasiriamali.”

Jambo jingine linalostahili kuhakikiwa na waandishi wa kiuchunguzi ni taarifa ya malipo ya madeni. Katika tamko la mwaka huu Zitto anatuambia:“NIMEPUNGUZA MADENI NILIYOKUWA NADAIWA TOKA TAMKO LA AWALI LA MWAKA 2015 NILILOTOA TAARIFA YA DENI KIASI CHA TSH 560,000,000/=”. Ukilirejea tamko la mwaka jana unakuta deni la NMB ambalo mwaka huu halipo, ikiashiria kwamba ameshalilipa lote. Ama? Pia tunakuta taarifa hii: “Nina mkopo wa Tshs. 24,624,046.88 katika Benki ya CRDB. Huu ni bakaa la mkopo wa Tsh. 200,000,000 niliouchukua mwaka 2010 na 2011.” Lakini mwaka huu tamko linasema ana deni la TZ 176,315,106.21 la CRDB. Je, hili ni deni la bakaa ile ile? Au ni mkopo mwingine? 
Deni la Taifa, kama alivyosisitiza Profesa Castel-Branco katika semina yetu kavazini, huchangiwa pia na mabenki ‘kukopesha madeni’. Huu ‘ufedhazishaji’ pia hupelekea madeni binafsi kugeuzwa kuwa madeni ya umma. Kwa nini? Kwa sababu taasisi za umma zilizokopesha watu binafsi zinapofilisika mzigo hubebwa na wananchi wote.

Badala ya kulindana tuanze kuanika madeni ya umma na kusisitiza wahusika walipe.

La sivyo tutakuwa hatuutendei haki #UhuruWaKujieleza.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 468

Trending Articles