Ripoti za CAG kuhusu Ubia wa NSSF na AZIMIO zinapingana?
Chambi Chachage
Nianze kwa kukiri kwamba mimi ni 'mshabiki' wa 'weledi' na 'ujasiri' wa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad. Japo hatufahamiani, nilivutiwa na umakini wake nilipokuwa namwona asubuhi kwenye kilima cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) akifanya mazoezi kwa umakini mkubwa. Alipoteuliwa kuwa CAG nilifurahi hasa baada ya kuyasikiliza mahojiano yake na Assumpta Massoi wa Radio ya Umoja wa Mataifa mwaka 2014. Katika mahojiano hayo alisema:
Ujasiri huo wa Profesa haukuishia huko 'nje'. Wakati wa sakata la Escrow, alinukuliwa na Shirika la Taifa la Habari (TBC) akisema:
Baada ya aliyekuwa Rais, Dakta Jakaya Mrisho Kikwete, kuagiza iwekwe wazi tuisome, wadadisi wa mambo tukatoa muhtasari wa 'Tuwaonao katika Ripoti ya CAG kuhusu Escrow'. Mjadala mkali uliozuka ulitufanya tuihoji iliyokuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kama CAG alilegeza kamba katika sakata la Escrow. Pamoja na hayo yote, niliendelea kuwa na imani na CAG.
Sasa umezuka tena mjadala mwingine mkali kuhusu ripoti ya uhakiki wa Shirika la Hifadhi ya Taifa (NSSF) uliofanywa na CAG. Msemaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Chiristopher Ole Sendeka, ameuchochea mjadala huu pale alipotoa tuhuma kali dhidi ya Mwenyekiti wa zamani wa PAC, Zitto Zuberi Kabwe. Lakini chanzo cha mjadala huu kuibuka upya ni mkutano wa NSSF na PAC, ambayo sasa inaongozwa na Naghenjwa Kaboyoka wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Mkurugenzi (mpya) wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara amekiri kuna utata na unashughulikiwa. Naye Mwenyekiti (mpya) wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Profesa Samwel Wangwe, naye amenukuliwa na gazeti la Serikali, Daily News, akisema mradi huo ulikuwa na walakini. Watetezi wa safu ya zamani ya NSSF kwenye mitandao ya jamii, nao wanadai kwamba hivi ni vita dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa NSSF, Dakta Ramadhani Kitwana Dau ambaye hivi karibuni ameteuliwa na Rais John Pombe Magufuli kuwa Balozi wetu nchini Malaysia.
Chama Cha ACT-Wazalendo nacho kimetoa tamko. Wadadisi wa mambo tumeshangaa ni kwa nini chama hicho makini tena chenye mshauri aliyebobea, Profesa Kitila Mkumbo, hakikumtumia Katibu Mwenezi wake mahiri, Ado Shaibu, kutoa tamko hilo. Badala yake tamko limetolewa na Habib Mchange ambaye Zitto Kabwe aliwahi kukiri "ndiye alikuwa CEO wa Leka Dutigite company." Kampuni hiyo ilifaidika kwa namna moja au nyingine na fedha kutoka katika mashirika ya Umma ya NSSF na la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Kwa wachambuzi wa masuala ya migogoro ya maslahi, kitendo cha huyo (aliyekuwa) Mkurugenzi wa Leka Dutigite kutoa matamshi yafuatayo kama Katibu wa Kamati ya Bunge na Serikali za Mitaa wa ACT-Wazalendo kunaibua maswali mengi kuliko majibu:
Tamko la kimaandishi 'lililowasilishwa' na Mchange linashangaza zaidi hasa ukizingatia haya maneno yake yanafanana na ya gazeti ambalo limekuwa likidaiwa kuandika taarifa nyingi za chama chao:
Ukaribu wa NSSF (wa enzi hizo) na baadhi ya vyombo vya Habari, wahariri na wanahabari siyo jambo jipya. Katika maadhimisho ya miaka 50 ya wadau wake mnamo mwaka 2014 huko Arusha, ripoti ya NSSF ilikuwa na haya ya kusema kuhusu mahusiano hayo:
Kama kuna mtu ambaye anapaswa kuzijua akaunti za NSSF kwa undani basi ni CAG. Kwa mujibu wa Taarifa za Mwaka za Hesabu za NSSF za mwaka 2010/2011, Profesa Assad alikuwa "Trustee" [Mdhamini]" wa NSSF ambaye alishiriki 'kupitisha' hesabu za shirika hilo baada ya kuhudhuria vikao vyote 12. Pia alikuwa mjumbe wa "The Finance and Investment Committee" [Kamati ya Fedha na Uwekezaji]" aliyehudhuria vikao vyote 4 bila kukosa. Taarifa kama hiyo ya mwaka 2005/2006 inaonesha uteuzi huo wa Profesa Assad ulianza lini na Wasifu wake wa Kitaaluma (CV) una muhtasari huu kuhusu yaliyokuwa majukumu yake kwa NSSF:
Kwa uzoefu huo, ni vigumu kuamini kwamba CAG hakuona shida yoyote katika hesabu za NSSF labda kama alikuwa na 'mgongano wa maslahi' kutokana na majukumu ya awali. Nadiriki kusema hivi kwa sababu "MANAGEMENT LETTER ON THE AUDIT OF FINANCIAL STATEMENTS OF NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) FOR THE YEAR ENDED 30 JUNE 2015" [Barua ye Menejimenti kuhusu Ukaguzi wa Hesabu za Shirika la Hifadhi ya Taifa (NSSF) kwa Mwaka Unaoisha Tarehe 30 Juni 2015] ya tarehe 17 Desemba 2015 itokanayo na ushirikiano wa kikaguzi na Wakaguzi wa Ernest & Young ina maneno haya nitakayoyatafsiri:
"The question here remains how a contract or agreement be signed and land ownership in a Public entity without agreed value of each piece of land? Also there was no verification and documents from Land Office provided that Azimio Housing Estate Limited owns 20,000 acres of land at Kigamboni for development. Therefore the signed agreement is not legal and void. Also the agreement was not vetted by the Attorney General (AG) which makes the matter more questionable...The audit scrutiny of such joint venture project revealed the following issues:...i. Overvalued price of Land to a tune of TZS 835,956,806 per Acre...ii. NSSF own land plot of 267 acres acquired for TZS 4,500,000...iii. The amount contributed by Azimio housing is questionable... iv. Financial capacity of Azimio Housing Estates Limited is questionable by having an issued and paid up share capital TZS 10,000,000...v. Lack of evidence for due diligence done with respect to Azimio Housing Limited and its affiliates...vi. NSSF awarded three tenders to owner of Azimio Housing Estates Limited who owns another Company called ZAK Solutions (Tanzania) Limited with tune of TZS 10,243,547,619.2... In addition, we were not availed with any documentation or title to substantiate that Azimio Housing Estates owns additional 19,700 acres of land.... [Swali linalobaki bila jibu ni jinsi mkataba au makubaliano yalivyosainiwa na umiliki wa ardhi na taasisi ya umma bila makubaliano kuhusu thamani ya kila kipande cha ardhi. Pia hakukuwa na uhakiki na taarifa katika Ofisi ya Ardhi inayotolewa kuonesha kuwa kampuni ya Azimio Housing Limited Estate inamiliki ekari 20,000 za ardhi Kigamboni kwa ajili ya kuendelezwa. Hivyo, mkataba uliosainiwa ni batili na haupo kisheria. Hali kadhalika mkataba huo haukupitiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) hivyo kulifanya suala hilo kuzidi kuwa tata. Ukaguzi wa mradi wa ubia umeibua masuala yafuatayo....i. Ardhi imethaminishwa kwa kiwango kikubwa mno cha TZS 835,956,806 kwa ekari...ii. NSSF inamiliki kitalu cha ardhi cha ekari 267 ambazo zilipatikana kwa TZS 4,500,000...iii. Kiwango ambacho Azimio Housing imekichangia kina utata...iv. Uwezo wa Kifedha wa Azimio Housing Estate Limited una utata ukizingatia imetoa na kulipa mtaji wa hisa wa TZS 10,000,000...v. Hakuna ushahidi unaoonesha kuwa Azimio Housing Limited na Washirika wake walifanyiwa uchunguzi ili kujiridhisha....vi. NSSF ilitoa zabuni tatu za TZS 10,243,547,619.2 kwa mmiliki wa Azimio Housing Limited ambaye pia anamiliki kampuni nyingine inayoitwa ZAK Solutions (Tanzania).... Zaidi ya hayo, hatukupewa taarifa au hati yoyote inayothibitisha kwamba Azimio Housing Estates inamiliki ekari 19,700 za ardhi za ziada]"
Wadadisi tunapata shida zaidi tunapoisoma 'RIPOTI YA MWAKA YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI KUHUSU UKAGUZI WA HESABU ZA MASHIRIKA YA UMMA KWA MWAKA WA FEDHA WA 2014/2015' ya tarehe 28 Machi 2016. Pengine kwa sababu siyo ripoti ya ukaguzi wa NSSF peke yake, humo hatuoni maneno yote yaliyopo kwenye hiyo ripoti ya CAG na Ernst & Young. Labda kwa sababu majibu mengine yalishapatikana katika kipindi hicho kifupi cha miezi mitatu ndiyo maana tunaliona tena suala hili hili lililokosa jibu:
Haya ndiyo masuala yanayohitaji ufafanuzi wa kina. Je, uhakiki wa wamiliki halisi wa AZIMIO na uwezo wao wa kiuwekezaji katika huo ubia wao na NSSF umeshafanyika? Na umiliki wao wa ardhi umethibitishwa? Kama yote haya bado hayajafanyika, wanufaikaji wa 'miradi' na 'nyumba' za NSSF wanapata wapi uwezo na utashi wa kudai kuwa eti CAG ameshahitimisha kwamba hakuna "shida" wala "ufisadi" katika mradi wa NSSF huko Rasi Dege, Kigamboni?
Isije ikawa ni aliyoyasema Profesa Assad: Ujasiriamali wa Kisiasa!