Quantcast
Channel: UDADISI
Viewing all articles
Browse latest Browse all 468

URITHI WA FIKRA

$
0
0
Na Isaack Mdindile

Nakumbuka kipindi nipo mdogo, siku nasherehekea kumbukumbu yangu ya kuzaliwa, kwa heka heka. Kwa shauku nilipendekeza kufanyike mabadiliko, kwamba tuachane na tuchane desturi ya kuzima mishumaa, maana kwa kuzima ni kama kuua miaka iliyopita na hivyo kubatiza liwe tendo la kusherehekea. Badala yake uwashwe mshumaa mmoja wa matumaini na usizimwe kamwe.

Kiumri, mdogo, na wakati ungali mfupi, lakini tayari niliwaza parefu kama Mwalimu Nyerere, ambaye katika moja ya hotuba zake aliwahi kunena: “Sisi tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau”. Nyakati nyeti kama hizi ukosefu wake ndio unasikika na unauma kwa umma zaidi. Ama kweli, We really miss Dear Mwalimu NyerereHow we wish you were here, kama alivyonena mshairi mmoja kwa lugha ya Kiingereza. 
Hakika, fikra zake mintarafu zilizosheheni fahari na faraja kipindi hiki njiapanda zinahitajika sana. Kidiplomasia, naona tunazidi kujenga kuta na kutu zaidi kuliko madaraja. Badala ya kuangalia mbele, tunajichungulia kitovu. Na kuja kwa ukoloni wa korona, kumefunua na kufukunyua uozo wa kiuongozi na ombwe zima la mfumo wa kibepari, katika kutubinafsisha, na kutugeuza mateja na mateka wa soko huria. Na labda, mbaya zaidi, kujificha nyuma ya pazia la uzalendo finyu.
Mara nyingi, jamii yoyote ile, inapojikuta njiapanda, hurudisha hamu na fahamu katika misingi/tunu zake. Ndio maana, sishangai tu kuona wengi tunakumbuka unabii wa Mwalimu Nyerere sasa, bali napongeza juhudi za udi na uvumba za kuleta maono yake adhimu mezani. Kongole, kwa wanabiografia Issa ShivjiSaida Yahya-Othman na Ng’wanza Kamata waliotoa kitabu adimu cha Development as Rebellion: A Biography of Julius Nyerere kinachovuma kupitia #NyerereBiography hivi karibuni. Binafsi, wakati nasubiria kukipata, nimeanza na kitabu cha Africa’s Liberation: The Legacy of Nyerere, kilichohaririwa na Chambi Chachage & Annar Cassam, ni maandiko mnato, yanasisimua. Tusitafuniwe kila kitu, kazi yetu sasa, iwe ni kusoma, kutafsiri, kutengenezea filamu na kueneza hadhira kwa wengi zaidi. 
Katika siku za hivi karibuni, moja ya jambo nimeshindwa kulimezea ni vifo vya ghafla bila faragha vinavyosababishwa na korona duniani, roho ya uchungu wa familia nyingi zinapokosa ibada ya kuaga, kuomboleza na kuzika wapendwa wao. Mbaya zaidi ni maziko ya halaiki. Hili ni pengo na pigo linalokosa maelezo.

Mzee Mgosi jirani yangu hapa kabla hajalazwa hospitalini aliamua kuandika wosia. Huu ndio urithi na mirathi kwa familia. Ni kile ambacho hakiozi wala kubanguliwa, na kinaendelea kutamadunishwa hata baada, lakini zaidi licha ya yeye kufariki dunia. Kifo kama kivuli hakikwepeki, taratibu kama kinyonga, kinanyemelea damu ya kila mwanadamu. Kwa hiyo, wosia ulikuwa kama cheche hai za mshumaa. Pamoja na udhaifu wake, bado ni aminifu mpaka mwisho. 

Sanjari na vitu alivyonavyo, hivyo havikuwa na umuhimu, alithamini na kuamini katika watu. Utu kama fikra ni hewa tuivutayo, havishikiki. Bila hivyo tunakufa! Alitambua kuwa vitu haviwezi kuzaa hekima wala kuleta furaha. Walakini, urithi kama utashi na furaha vinatoka ndani, havionji kifo, vinadumu milele:  mzee alitaka kuendelea kuwa hai katika maisha ya wale watakaokunywa na kula fikra zake.

Tazama, urithi za huyu Mzee ni kama ule wa Mwalimu Nyerere, ambao ni upevu wa fikra zake, kuliko utawala wake. Kuacha fikra kama urithi, ni kama kufuru na wazo fukara sana. Naam, wakati anaandika wosia juu ya taifa letu, alijifananisha na mshumaa, kwa unyenyekevu bila kujimwambafai. 

Na hapa ndipo wengi hatumwelewi. Hivyo, taratibu bila aibu, tunazima mshumaa wa MwalimuNyerere, kumfanya mzimu katika mapango ya kale. Kama hilo halitoshi, tuliishia kuweka mkato, katika mchakato wa Katiba mpya licha ya kugharimu rasilimali nyingi za umma. Nini kinatukwaza kumalizia huu mchakato?

Kuhusu fikra nadra za Mwalimu Nyerere, Profesa Shivji anasema kwamba tunaweza kuziweka katika mafiga matatu: usawa na utu, umoja wa kitaifa na azimio na uongozi. Ni utatu mtakatifu. Pamoja na madoa ya muungano, zimeunganikana kama bara na visiwani.

 Inashangaza kwamba, leo hii tunajipambanua kujenga vitu, kuendesha taifa kiilani kuliko kikatiba, kubaguana kivyama na hata kudiriki kutetea uongozi mbovu. Bila dira tumejawa na hila. Tunapoteza nguvu na fedha tena za umma katika kuongeza wanachama, kuunga mkono juhudi za mwenye vitu kuliko kujenga nchi. 

Ndio maana, kila uchao Watanzania wengi hawavutiwi na siasa za vyama vya siasa. Hali ya kutishiana inazidi, na siasa zinapwaya, zinapauka kama sio kupwayuka.

Tujisahihishe!Tuache ukuku na ukondoo. Tuamshane kutoka usingizini, katika usingizi wa mawazo mgando.
Kabila la wanasiasa wengi wanajificha nyuma ya pazia la Mwalimu Nyerere, wakimtumia na kuficha agenda zao binafsi au za kichama. Suala na swali la muhimu kwa sasa ni kuwekeza katika kuwawezesha na kuwainua wananchi. Kwa maana ya kuimarisha umoja na harakati za wafanyabiashara, wakulima, wafugaji na wafanyakazi ambao wengi wao bado ni wavujajasho, pamoja kuongeza uelewa na udadisi katika mambo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Haya ni makundi muhimu na ni katika hayo  ambapo ujinga, umaskini, vinageuka kuwa taji na mtaji wa wanasiasa.

Pamoja na mapungufu ya zama zake, Mwalimu Nyerere ni zaidi ya jina. Ni utambulisho na urithi wa nchi katika ncha zote duniani. Fikra zake tunduizi zilijaribu kusitiri na kutafsiri falsafa zetu za Kitanzania na Kiafrika kwa ujumla, hasa kwenye uongozi bora, uhuru wa fikra, na maendeleo ya kweli. Lengo na sababu ya uwepo wa serikali ni kutumikia wananchi na kuleta ustawi stahiki wa jamii. Huo ndio urithi wa kweli wa kifikra na kimaendeleo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 468

Trending Articles