Lengo la waraka huu ni kukupasha yaliyojiri huku duniani tangu ulipotangulia mbele za haki mnamo Jumamosi ya Aprili 25, 2020.
Twazidi kumuomba Allah S.W akuondoshee adhabu ya kaburi wewe na marehemu wetu wote, awasamehe dhambi zenu, na awajaalie pepo (Jannatul Firdaus)
Tumehuzunika sana. Kifo chako kimefanana na cha marehemu mama yako, bibi yetu mpendwa Lahiu (Allah S.W amrehemu) aliefariki dunia na kuzikwa na Serikali wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa tauni (plague) mwaka 1980, japokuwa yeye alikuwa na dalili za kipindupindu.
Tunatambua ulifikwa na umauti ukiwa katika hali ya wasiwasi na taharuki kubwa. Wapwa zako walituelezea namna ulivyobugujikwa machozi ukiwasihi wauguzi wakusaidie dhidi ya maradhi ya shinikizo la damu/presha ulokuwa nayo badala ya kukupeleka kwenye kituo cha ugonjwa wa homa kali ya mapafu uletwao na virusi vya korona, yaani COVID-19(Sambaani twasema koona). Wakati ukiwa kwenye karantini, ulipoteza fahamu, moyo wako ulikoma mapigo, pumzi yako ikakata, na mauti yakakufika. Inna Lillah wa inna illayhi raji’un!
Tulitamani tukakuzike Sambaani kwa taratibu zetu za Kiislam, Kisambaa na Kipare. Haikuthibitishwa kama ulifariki dunia kwa koona: tulifahamishwa kuwa matokeo ya sampuli yako “hayaeleweki.” Licha ya hivyo, ulizikwa kwa uliokuwa utaratibu wa Serikali. Tulipata faraja kidogo tulipokumbushana kuwa wakati wa uhai uliwahi kusema kuwa, utakapofariki dunia uzikwe popote panapostahili ili kupunguza usumbufu na gharama kwa tuliobaki hai.
Ikawadia siku ya maziko. Ndugu zetu walikamilisha kuchimba kaburi majira ya ya saa nne asubuhi. Serikali ndio waliitayarisha maiti yako. Hatuna hakika kama ulikafiniwa kwa taratibu za imani yetu ya Kiislam. Kwa wafungaji, Magharib (muda wa kufturu) uliwakutia makaburini, wakafungua swaum huku wakingoja maiti yako. Takribani mishale ya saa tatu kasoro usiku, maiti yako ilifikishwa makaburini, na kila kitu kilitakiwa kufanyika kwa haraka.
Hali ya mawingu ilisababisha giza nene eneo lile. Mvua ilinyesha, baridi ilizizima na vichaka eneo la makaburini viliogofya. Ndugu na jamaa walitumia mwangaza wa simu zao za mkononi kuthibitisha kuwa kweli ile ni maiti yako kabla ya kuendelea na maziko. Basi wakajipanga kwa haraka haraka angalau wakafanikiwa kuiswalia maiti yako kabla ya kutiwa kaburini. Tukamaliza hilo kwa salama. Alhamdulillah!
Sasa nikueleze kwa uchache yaliyojiri baada ya hapo.
Ndugu na jamaa tulipashana habari ya kifo chako. Namna kifo chako kilivyotokea ilihuzunisha na kuogopesha wengi. Habari ilisambaa kama wasambaa katika milima ya Usambaa. Tulikaribishwa kuzungumzia kifo chako kwenye chombo cha habari cha kimataifa cha BBC. Tulijiuliza kama ni sahihi kwenda kuanika madhila yako kwa ulimwengu mzima.
Tunaamini katika al-Qadar ya Allah S.W, kwamba kheir na shari zote hutoka kwake na kwamba kila chenye uhai hatimaye kitauonja umauti. Haja gani basi kupaza sauti ilhali mauti yashakufika kama ilivyoandikwa. Baadhi walikuwa na hofu kuwa inaweza kuonekana kana kwamba tunakiuka maelekezo ya Serikali juu ya utoaji habari za koona. Lakini majibu ya kipimo chako hayaeleweki, hatujui kama ni koona ama la.
Wengine wakasema siku zote kifo ni fursa maridhawa kwa waja kukumbushana wajibu wetu. Basi ndugu tukaridhia kufanya mahojiano kugusia maeneo matatu.
Mosi, ni kuhakikisha kuwa watu wenye maradhi mengine mbali na koona wanaendelea kupata huduma kwenye vituo vya afya bila ya kuwa na hofu. Pili, bila kuhatarisha afya zao na za wengine, ndugu waruhusiwe kuwazika marehemu wao kwa heshima kwa kuzingatia mila na desturi zao. Na tatu, vipimo vya koona viongezwe ubora ili kuondoa hali ya sintofahamu na taharuki.
Ni juma moja limetimia tangu ulipotutoka mpendwa shangazi. Ndani ya muda huu mfupi, kumekuwa na mwitikio wa Serikali na wananchi kwenye maeneo hayo matatu.
Japokuwa sijajaaliwa kuona mwongozo kuhusu swala la kwanza, lakini jamaa zetu kadhaa wanaohudumu kwenye sekta ya afya wanasema kuwa msisitizo umetolewa kuhakikisha kuwa watu wenye maradhi mengine wanaendelea kupata huduma kwenye vituo vya afya. Hii itasaidia kuondoa wasiwasi uliokuwa unaanza kujengeka hasa kwa wale ambao wanahitaji huduma hizo mara kwa mara.
Wifi yako, yaani mama yangu mzazi, aliingiwa na hofu ya kwenda hospitali kupimwa macho na kupatiwa dawa. Baada ya kumnasihi alikubali nikamsindikiza kwenda Mloganzila, akahudumiwa vizuri na kupatiwa dawa za kumtosheleza kwa miezi mitatu. Alistaajabu kuona idadi ndogo sana ya wagonjwa waliokuwepo pale siku hiyo. Alisema kipindi cha nyuma, imewahi kumchukua siku nzima kupata huduma lakini mara hii haikuzidi hata saa moja. Hatukuweza kufahamu kama ni ufanisi umeongezwa ama ni wasiwasi ndio ulisababisha wagonjwa wachache tu kwenda hospitali siku hiyo.
Kwenye eneo la pili, Serikali imeelekeza wahusika wawezeshe kufanya mazishi kwa heshima zote na utu, na kwamba “WIZARA INAELEKEZA HAKUNA SABABU YA MAITI ZA WAPENDWA WETU WALIOFARIKI KWA UGONJWA WOWOTE ULE, KUZIKWA AU GIZANI.” Ni imani yangu mwongozo huu umezingatia kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizosababisha maziko kufanyika usiku.
Wakati wa maziko yako, tulielezwa kwamba maiti (ikiwemo ya kwako) zilichelewa kwa sababu baadhi ya makaburi hayakuchimbwa kwa wakati na ndugu wa marehemu hawakupata taarifa mapema. Lakini pia, binamu zangu walitueleza kuwa maafisa wachache waliokuwa wanaishughulikia miili yenu walionekana dhahiri kuwa wameelemewa na kazi ile. Shangazi, nitawashauri wahusika washughulikie changamoto hizi ili tuwazike marehemu wetu kwa utu na heshima huku tukizuia maambukizi zaidi ya koona na magonjwa mengine.
Nimeona jitihada kwenye eneo la tatu pia: kuongeza ubora na umakini wa vipimo vya koona. Shangazi, siku ya Jumapili tarehe 3 mwezi Mei, 2020, ikiwa ni siku saba kamili tangu tupigwe butwaa ya kuambiwa majibu ya kipimo chako hayaeleweki, Mheshimiwa Rais alihutubia na kugusia suala hilo kwa kina. Shauku yetu ilikuwa juu sana tukitaka kufahamu nini mikakati ya serikali katika eneo hili.
Kwa kifupi, Mheshimiwa Rais alituambia kuwa walifanya zoezi la kutathmini umakini wa maabara katika kupima koona. Walitumia sampuli za binadamu na sampuli za majaribio toka kwenye matunda kama funesi (huku mjini wanaita fenesi), kwa wanyama kama ngoto (kondoo) na ndege kama kware. Na kwamba majibu yalikuwa aina nne: hasi (negative), chanya (positive), yasiyoeleweka (inconclusive) na yasiothibitika (indeterminate). Kiukweli, shangazi sisi hatujui kama tufarijike au tuhuzunike na maelezo haya. Tupo tupo tu na butwaa yetu.
Basi baada ya hotuba ya Mheshimiwa Rais pamekuwa na mijadala mikali kila kona. Shangazi, hebu fikiria (sijui kama unaweza kufikiria huko uliko), eti sampuli ya funesi imetoa matokeo yasioleweka (inconclusive) kama tulivyoelezwa kuhusu matokeo ya kipimo cha sampuli yako. Mpwao mmoja alilalama kwa uchungu, yaani badala wangerudia kipimo cha shangazi yetu ili kieleweke, wao wanachezea vipimo kupima funesi.
Wataalam mbalimbali wa masuala ya maabara wametoa maoni tofauti tofauti. Kuna wanaohoji uhalali wa kutumia sampuli toka kwa wanyama, matunda na “oili” (mavuta ya gai kama tusemavyo Sambaani) katika zoezi hilo. Wengine wameshangaa kupitia makundi sogozi (WhatsApp) kuwa inawezekanaje maabara ikashindwa kutofautisha sampuli za binadamu dhidi ya zile zisokuwa za binadamu. Kuna wanaojiuliza, je ukusanyaji na uwasilishaji wa sampuli za kichunguzi ulizingatia protokali za maabara? Cha muhimu ni pande zote kuheshimu na kuvumilia mtazamo wa pande nyingine ili kuwa na mjadala wenye tija.
Wengine wamefanya ubunifu wa kusambaza picha za mbuzi waliovalishwa barakoa na mipapai iliokatwa kwenye mitandao ya kijamii. Alimradi kumekuwa na hoja na vihoja. Kiujumla imani kwa vipimo vya maabara inapungua.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais inaashiria amekusudia kujiridhisha na uhalali na umakini wa vipimo vya maabara. Amesisitiza mara kadhaa kwamba hivi ni vita na wanaweza kutumika watu au vifaa kutuhujumu. Siku moja baada ya hotuba ya Rais, Waziri wa Afya ameunda kamati ya wataalam wabobezi kuchunguza mwenendo wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii na amemwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuwasimamisha kazi mara moja Mkurugenzi na Meneja Udhibiti wa Maabara tajwa ili kupisha uchunguzi.
Shangazi, naamini uchunguzi huu ungefuatia mara tu baada ya sampuli za matunda na wanyama kabla ya hotuba ya Rais walau taharuki niliyoiona kwenye mitandao ya kijamii isingekuwa kwa kiwango hicho. Nataka kuamini Serikali imeweka utaratibu wa vipimo makini wakati uchunguzi ukiendelea. Siku za baadae tutaweza kuchambua athari (chanya na hasi) za uchunguzi huu wakati mlipuko wa koona ukiendelea.
Mpendwa shangazi, kuna wachangiaji mada ambao wamediriki kuwalaumu watendaji wa maabara. Wataalam wa saikolojia wanasema ni kawaida kwa wanadamu kulaumu mtu au kitu pindi tufikwapo na majanga. Si haba, lawama yasaidia kupunguza machungu. Lakini ukiwa upande wa kulaumiwa hakika inauma.
Shangazi, ni dhahiri kabisa kuwa lawama kwa watendaji wa maabara zinaweza kuwavunja moyo katika kazi yao muhimu na pia kusababisha wasiwasi juu ya mustakabali wao. Nafikiria kuwasihi wadau wasiendelee kuwalaumu wapimaji, kabla uchunguzi wa kina kukamilika. Siku zote, utambuzi wa tatizo ni hatua muhimu sana kufikia ufumbuzi mzuri wa tatizo husika.
Shangazi yangu, sisi ukoo ambao tunafika mia kadhaa ni miongoni mwa maelfu ya watumiaji wa huduma hizi muhimu. Tuna mengi ya kuchangia katika uimarishaji wa hizo huduma. Lakini tukiwaza haya matangazo ya mara kwa mara kutoka kwenye Mamlaka ya Kudhibiti Mawasiliano Nchini Tanzania (TCRA) na matukio ya baadhi ya watu kushitakiwa kwa sheria hizo, basi tunaingiwa na hofu na tunanyamaza.
Nimekuandikia waraka huu kukufahamisha, japo kwa uchache yaliyojiri tangu ulipoaga dunia. Nimegusia jitihada zinazoendelea katika maeneo matatu: kuhakikisha vituo vya afya ni salama kwa wagonjwa wote, kuwezesha maziko yenye utu na heshima, na kuimarisha vipimo vya koona. Mie mpwao nina imani jitihada hizi zitaendelea ili wengine wasipatwe na madhila kama yako na jamaa zao waepushwe na hekaheka tuliyokabiliana nayo baada ya kifo chako.
Na sisi twazidi kumuomba Allah S.W atujaalie mwisho mwema na tuzidi kuwa Wacha Mungu wenye kumsujudia na kumhimidia yeye pekee.
Allah S.W azidi kukurehemu shangazi yetu mpendwa na panapo uhai nitakuandikia tena, In sha Allah.
Wakatabahu.
Pumzika kwa salama na amani shangazi yangu.
Amin.