Na Zuhura Yunus
“Mahiga wetu”. Huu ndio ujumbe wa mwanzo niliousoma kupitia simu yangu pindi tu nilipoamka. Si kawaida kwa Mariam Omar tunayefanya kazi pamoja BBC Swahili kuniandikia mapema namna hiyo. Na kauli yake hiyo ndio kabisa hasa katika kipindi hiki cha taharuki ya janga la korona nchini. Tayari moyo ulianza kunidunda na kichwani najiambia hapana, haiwezekani. Kajuaje, nani kamwambia na maswali chungu nzima.
Nikajipa moyo. Kisha nikaendelea kutazama na kuona ujumbe wa Halima Nyanza ambaye naye yuko BBC, ofisi za Dar es Salaam. Kufungua nikakutana na taarifa rasmi ya serikali ya Tanzania ikisema Balozi Mahiga hatunaye tena. Hapo ndipo niliinuka kama nilopigwa mkwaju.
Swali la kwanza nilijiuliza mara ya mwisho ‘tulimsumbua’ lini tukitaka mahojiano naye. Na ndilo jambo ambalo karibia asilimia 70 ya mkutano wetu tulokuwa tukiandaa matangazo yetu ya Dira ya Dunia TV ndicho tulichojadili. Tukikumbushana namna rafiki yetu Mahiga alivyokuwa mwepesi tukimtafuta. Kwenye kila chombo cha habari tunajua kiongozi gani mwepesi kupatikana na nani atatula unga wa roho.
Balozi Mahiga yeye ni miongoni mwa viongozi ambao hatukatalii mahojiano hata siku moja. Ikimbidi kutoa udhuru basi atatumia diplomasia ilotukuka mpaka mwenyewe utakubali. Sidhani kama kuna mwandishi yoyote wa habari ambaye anathubutu kusema kiongozi huyu alikuwa msumbufu ukitaka mahojiano naye.
Jambo ambalo lilizidi kutufanya tumthamini Balozi Mahiga ni wakati tunataka kuzindua kipindi chetu cha TV, Dira ya Dunia, miaka minane iliyopita. Tulikuwa tukipata mafunzo takriban miezi sita. Hata hivyo miezi mitatu kabla ya kuzindua rasmi tulikuwa tukifanya matangazo yote kama vile kweli tunaenda hewani japo siyo, na ilitubidi tutafute wachambuzi na viongozi halisi tuwahoji.
Huwezi amini Balozi Mahiga tulimweleza wazi kuwa ni majaribio tu ila kwa muda wa miezi hiyo mitatu tumemsumbua tukimhoji kama tuko mubashara. Na hapo si kipindi chetu tu bali pia kipindi dada cha Kiingereza, Focus on Africa. Na wakati huo ifahamike hakuwa katika nafasi ndogo hata kidogo duniani. Alikuwa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia akikaa Marekani wakati huo. Hapo tukipishana saa nyingi baina ya Uingereza na Marekani ila hakusita hata siku moja kutusaidia.
Bila shaka alikuwa ni kiongozi aliyeamini kuwa ana wajibu kwa wananchi na dunia kwa jumla. Wakati akiwa na wadhifa wa uwaziri wa mambo ya nje wa Tanzania, wenzetu wa Idhaa ya Kiingereza ya Focus on Africa walikuja kwetu kutaka tuwasaidie kumpata Balozi Mahiga. Tulifanya hima na kama ilivyo ada aliipokea simu yetu. Tukamfahamisha tulichohitaji ila akasema ana safari ya Addis Ababa hivyo anawahi uwanja wa ndege kuelekea huko. Wazo letu la awali ilikuwa aende ofisi zetu za Dar es Salaam lakini kutokana na muda basi tukamsihi atumie Skype.
Waziri Mahiga hata hakufikiria mara mbili mbili kama ilivyo kwa baadhi ya viongozi wanaosita sita kuhojiwa. Akamwomba msaidizi wake amsaidie mpaka tufanikishe. Tuliweza kumpata dakika ya mwisho japo hakuonekana vyema kwani sura yake ilikatwa nusu ila alisikika vyema. Kwa umuhimu wa taarifa yenyewe wenzetu walishukuru na kuitumia hivyo hivyo kama ilivyo.
Wakati bado akiwa waziri wa mambo ya nje kuna wakati alihudhuria mkutano wa makubaliano ya kuwa na Eneo la Biashara Huria Barani Afrika (CFTA). Mkutano huo ulikuwa ukijadili namna Waafrika wangeweza kufanya biashara huru na mipaka iwekwe wazi miongoni mwa nchi za Afrika. Tukaona ni fursa nzuri ya kuzungumza na Balozi Mahiga akiwa nchi ulipofanyika mkutano huo, Rwanda. Mwenzangu, Zawadi Machibya, ndiye alikuwa akisimamia uandaaji wa taarifa ya mkutano huo kwa ajili ya kipindi hicho cha TV cha Dira ya Dunia akiwa na jukumu la kuhakikisha tunakuwa naye hewani. Kiongozi huyo alokuwa na hadhi ya kipekee alihangaika sana kuunganisha Skype ila, kila akijitahidi wapi.
Kwa bahati mbaya, licha ya jitihada zote hizo hatukufanikiwa kwenda naye hewani kutokana na changamoto za kiteknolojia. Alikuwa na subra ya ajabu. Wala hakuhamaki kwa usumbufu huo. Hata baada ya hapo bado aliendelea kushirikiana nasi licha ya mshikemshike wote huo. Huyo ndio Balozi Mahiga.
Mwezi Agosti 2014, chini ya Mhariri Mkuu wakati huo katika ofisi za Dar es Salaam, Hassan Mhelela tulizindua kipindi cha Amka na BBC. Ndio ilikuwa mara ya kwanza kipindi hicho cha asubuhi cha redio kurushwa mubashara kutoka jijini Dar es Salaam. Mimi na mtangazaji mwenzangu Salim Kikeke tulitoka Uingereza kuja kujiunga na wenzetu katika uzinduzi huo. Salim alikuwa mshereheshaji siku hiyo nami nikawa mtangazaji nikishirikiana na Baruan Muhuza (Sasa yuko Azam TV) kurusha matangazo hayo siku ya uzinduzi.
Kwa kuwa tulifika Dar es Salaam siku chache kabla ya shughuli hiyo, nilipewa kadi za mwaliko niwapelekee baadhi ya wachambuzi na viongozi tunaowatumia sana kwenye matangazo. Balozi Mahiga alikuwa mmojawao. Wengine walikuwa ni pamoja na Dakta Salim Ahmed Salim na Profesa Ibrahim Lipumba. Licha ya kuwakabidhi dakika za mwisho, waliupokea vyema mwaliko huo na kushiriki kikamilifu.
Kama nilivyosema awali uzoefu, upeo, kujua wajibu wake, heshima na kuwa mtu muwazi labda ndizo sifa zilizomfanya asiwe akitukatalia kuhojiwa. Kuelekea mwishoni mwa mwaka 2019, ilitolewa ripoti na Shirika la Kimataifa la kutetea Haki za Binadamu lijulikanalo kama Human Rights Watch (HRW) ambalo liliishutumu Tanzania kwa ukandamizaji wa vyombo vya habari. Tulijua wazi kuwa kwa namna Tanzania ilivyo kwa sasa, kupata kiongozi wa serikali kuzungumzia jambo lolote ni mtihani, sikwambii tena tuhuma ndio kabisa. Ila baada ya kujadiliana na Wazir Khamsin ambaye kwa siku hiyo ndiye alikuwa mtayarishaji wa taarifa hiyo, nikaamua kumpigia Balozi Mahiga. Wakati huo alishabadilishiwa wizara.
Nilipompata nikamfahamisha kuwa nawasha spika ya simu ili na Khamsin naye apate kumsikia. Kwa uzoefu wetu ingekuwa kiongozi mwengine jibu ambalo tungelitarajia basi vichwa vingeuma. Ila Waziri huyu wa Sheria na Katiba akanisikiliza kisha akanijibu kama ifuatavyo “Hili ni suala zito linalohitaji kushauriana kwa upana zaidi kabla sijatoa taarifa.”
Kawaida habari ikitoka nasi kwa kazi zetu ni wajibu kupata jibu siku hiyo hiyo. Lakini kwa kuwa tulijua si mtu ambaye angeweza kutukatalia kusudi tuliheshimu maelezo yake. Ila tulimwuuliza, je tunaweza kukunukuu hewani na jibu hilo? Akasema, naam, tunaweza kumnukuu kwani ndio kwanza ripoti ilikuwa imemfikia na alihitaji muda awasiliane na wenzake ndiyo angejibu. Jambo ambalo tuliridhia. Huyo ndie Balozi Mahiga.
Binafsi nilimwona ni mtu muungwana, mwenye sauti ya upole, mwenye ufahamu na elimu iliyosheheni, mstaarabu na mwanadiplomasia aliyebobea. Ni nadra kupata kiongozi mwenye sifa hizi na hasa aliye madarakani mwenye utayari wakati wowote kutukabili sisi wanahabari. Hakika alikuwa rafiki wa waandishi wa habari.
Natoa pole zangu nyingi kwa familia yake na huku nikijua maumivu ya kumpoteza ni makubwa mno. Nasi tumempoteza mtu muhimu kwetu. Naam ni Mahiga wetu – Rafiki yetu.