Quantcast
Channel: UDADISI
Viewing all articles
Browse latest Browse all 468

Karata ya Mwisho ya Maalim Seif?

$
0
0

Chambi Chachage

@udadisi

 

Jaramogi Oginga Odinga. Morgan Tsvangirai. Raila Odinga. Michael Sata. Kizza Besigye. Seif Sharif Hamad. Wanasiasa hawa wana kitu kinachofanana. Harakati za muda mrefu za kuwania Urais. Lakini ni mmoja tu aliyefanikiwa. Wapo wanaoendelea na jitihada, wengine wametutoka. Mmojawao inasemekana aliwahi hata kuomba kuwa Rais kwa muda mfupi tu aitimize ndoto yake.

 

Maalim Seif kama anavyojulikana na wengi ameamua kutokata tamaa. Baada ya kugombania nafasi ya Urais wa Zanzibar mara  tano, nguli huyo wa siasa za Tanzania hasa za upande wa visiwa vya Unguja na Pemba ameamua kujaribu tena mwaka huu wa 2020. Akiwa na miaka 77, Maalim siyo tena yule kijana ngangari aliyewapa taabu Marais wastaafu wa Zanzibar aliogombania nao enzi hizo za miaka ya 1995 na 2000, akina Salmin Amour ‘Komandoo’ na Amani Abeid Karume. 

Lakini kama kweli uzee ni dhahabu basi Maalim ni dhahabu iliyopitishwa kwenye tanuru kali la moto wa siasa za upinzani nchini na kutoka ikiwa dhahabu kweli kweli. Na ndiyo maana chama cha ACT-Wazalendo na kiongozi wao wa chama, Zitto Kabwe, wana kila haki ya kujisifu kwa kuweza kumpata na kumsimamisha. Waliyempata siyo mgombea tu, bali mwalimu hasa wa siasa.

 

Changamoto kubwa iliyo mbele yao sasa ni kufanikisha kila kilichowashinda akina Odinga kule Kenya, Besigye kule Uganda, na Tsvangirai kule Zimbabwe. Yaani kufanya kile alichofanya Sata kule Zambia. Ila lahaula Zambia siyo Tanzania. Ina historia na utamaduni wa wapinzani kushinda.

Ili kuwa sahihi zaidi, Zambia imeshazoea wagombea Urais wa vyama vya upinzani kushinda na kutangazwa kuwa wameshinda. Lakini siyo Zanzibar. Mwaka 2015 ilibidi hata matokeo yafutwe. 

Sasa, je, mwaka huu itakuwa tofauti? Mvumulivu Maalim ameamua na kutoa tahadhari kuwa safari hii hatazuia wafuasi wake kuamua watakachoamua kama atafanyiwa figisu figisu, yaani hujuma. Wapo wanaoona ni kitisho. Ila ni tahadhari tu. Kutukumbusha madhila ya mwaka 2000.

 

Kwa maana nyingine, kiongozi wa kisiasa mwenye ushawishi mkubwa Zanzibar pengine kuliko wanasiasa wote amesema sasa basi. Imetosha. Mstahimilivu Maalim kaamua sasa liwalo na liwe.

Wadadisi wa mambo tunaona hii ni ishara kuwa amebakiwa na karata moja tu tena ya turufu. Na ameamua kuicheza vilivyo karata yake hiyo mwisho. Kama ni kuwa Waziri Kiongozi si ameshakuwa. Na kama ni kuwa Makamu wa Rais si ameshakuwa. Hivyo, kilichobaki ni Urais tu.

 

Hali hii inaweza kumweka njiapanda kiongozi wa chama chao, Mwami Zitto, ambaye naye azma yake ni kuwa Rais siku moja, pengine mwaka 2025 maana mwaka huu nyota ya jaa ya kambi ya upinzani Tanzania inamuangazia mgombea kupitia tiketi ya CHADEMA, Tundu Lissu. Mahesabu ya kimkakati yanaonesha kuwa subira yaweza kuleta heri hasa ukizingatia ugumu wa uchaguzi huu ambao ni dhidi ya Rais aliyepo madarakani, yaani John Magufuli. Kwa mantiki hiyo, kumsimamisha Bernard Membe agombee Urais Tanzania ni mbinu tu ya masafa marefu kisiasa.

Chama kichanga kilichokuwa kinasuasua kisiasa kwa hakika kimehuishwa kwa ujio wa Maalim Seif na kundi lake kutoka kwenye chama cha CUF baada ya mtafaruku na kundi la Profesa Ibrahim Lipumba. Hivyo, kwa ACT-Wazalendo hata kupata tu fursa ya kuwa sehemu ya kuunda Serikali ya “Umoja wa Kitaifa” pamoja na CCM, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, itakuwa ni mafanikio makubwa baada ya kuiongoza Manispaa ya Ujiji. Lakini hilo halitawezekana kama ambavyo halikuwezekana mwaka 2015 iwapo Maalim Seif atakataa kata kata kuwa tena Makamu wa Rais. 

 

Pengine litawezekana kama CCM itatuonesha maajabu kwa kukubali Rais wa Zanzibar atoke chama pinzani. Ila wajuzi wa mambo watakuambia hiyo ni ndoto ya Alinacha. Tena watasisitiza kuwa bila CCM hakuna “Mapinduzi Daima” Zanzibar achilia mbali Muungano na ‘Tanganyika’. 

Vyovyote itakavyokuwa, kilicho muhimu ni kuhakikisha kuwa watu hawapotezi tena maisha yao kama ilivyokuwa mwaka 2000. Ni kweli mabadiliko na demokrasia ina gharama zake. Ila uhai ni ghali. Wala hauna gharama. Atakayeshinda Urais aachiwe tu awe Rais na watu waendelee kuishi.

 

Daima muungano usio wa dhati na hiari haudumu. Tujenge udhati na uhiari. Urais huja na kupita.


Viewing all articles
Browse latest Browse all 468

Trending Articles