Kutumbuliwa Kwa Kitwanga Kunaashiria Kitu Kipi?
Chambi Chachage
Uamuzi wa Rais Magufuli kutengua uteuzi wa (aliyekuwa) Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, umepokelewa kwa msisimko katika mitandao ya jamii. "Hii", anadai Mtanzania mmoja katika Twitter, "haijawahi tokea tangu Tanzania iumbwe". Mhariri mfawidhi wa gazeti maarufu anaungana naye kwa kusema "Haijapata kutokea. Namba inasomeka kila kona #Tanzania".
Mtetezi wa mchakato wa kuwapima watu kiuchunguzi kabla ya uteuzi wao (vetting) anasisitiza kwamba kilicho muhimu ni 'tiba'. Naye mwandishi mahiri wa vitabu vya 'ushushushu'amempongeza Mtumbua Majipu kwa 'kutwanga' baada ya kilio chetu 'kumbipu'.
Hata mwanasiasa machachari na mbunge pekee wa chama kinachochipukia kwa kasi cha ACT-Wazalendo naye kaguswa:
Hakika Rais anastahili pongezi nyingi. 'Tusimbanie'. Hongera sana!
Wakati tunaendelea kumpongeza pia tukumbuke 'hapa kazi tu' kwa wanahistoria ni kuyafukuafukua makabrasha ili kujaribu kuelewa tumetokea wapi katika masuala fulani, tupo wapi na tunaelekea wapi ili tusije tukayarudia (makosa) yale yale kiuwendawazimu.
Historia ya kisiasa inaturudisha kwenye kampeni za uchaguzi za mwaka 2015. Pale tunakutana na maneno haya ya Magufuli:
Kwa wafuatiliaji wa kila kichesemwacho watakumbuka kuwa hata baada ya kuwa Rais, Magufuli alinena maneno kama hayo kuhusu wateule wake wengine alipokuwa akihutubia pale Kinyerezi:
Mbinu hii ya uteuzi na utetezi ni ya aina yake. Inaleta ugumu na ukakasi hasa kwa wadadisi wanaotaka kujua vigezo vyote ambavyo Rais wetu hutumia katika kuteua. Tukumbuke mwaka jana Udadisi iliwahi kuhoji majibu yafuatayo ya Rais na haki yetu ya kikatiba ya kupata habari/taarifa kuhusu masuala muhimu ya nchi yetu pale wanahabari walipojaribu kuhoji mantiki ya idadi ya manaibu waziri kwa kuzingatia uunganishaji wa wizara na vigezo vilivyotumika kuwarudisha mawaziri kadhaa kutoka kwenye Baraza lililopita:
Baada ya kashfa nzito ya Lugumi kuibuliwa na mti wa Kitwanga kupondwa mawe na wapinzani, tumekuwa tunajiuliza kama vigezo vyote vya 'vetting' vilizingatiwa ilikuwaje akateuliwa kuwa Waziri na Mkombozi wetu wa kupambana na ufisadi nchini? Tunaoamini kuwa wanasiasa wa 'mjengoni' Dodoma wanajuana kwa vilemba, maneno haya aliyoaandika aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) yalituacha mdomo wazi:
Lakini cha ajabu zaidi mnamo mwaka jana mtandao unaopigwa vita (na mafisadi) wa Jamii Forum ulitumika kuweka maneno haya:
Je, 'vetting' haikuziona ishara hizo za nyakati? Kama haikuziona, hata Mungu wa Magufuli hakuyaona yote haya? Sikio lake la yeye awekaye na aondoaye watawala ni zito hadi asisikie maombi hayo?
Mwisho kabisa historia yetu inatukumbusha kwamba Rais wa awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alipigiwa kelele asiteue baadhi ya watu lakini akawateua tu. Matokeo yake Baraza la Mawaziri likavunjwa baada ya miaka miwili tu tena baada ya fedha nyingi kutumika kuwafanyia semina elekezi mawaziri kwenye hoteli ya kihafahari ya Ngurdoto. Kwa miaka kumi kazi kubwa ikawa ni kuweka/kuziba viraka ambapo katika Wizara moja tu mawaziri walibadilishwa zaidi ya mara tatu - kutoka kwa Naziri Karamagi kwenda kwa Ibrahim Msabaha kisha kwa William Ngeleja halafu Sospeter Muhongo hadi George Simbachewene - na Waziri wake mmojawapo, Shukuru Kawambwa, alihamishwa zaidi ya mara tatu.
Gazeti la Mwananchi linatukumbusha kwa miaka 10 Serikali hiyo ya 'Ari Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpya ('ANGUKA') na 'maisha bora kwa kila Mtanzania' ikaishia kutumikiwa na"mawaziri 120" huku JK akitema "mawaziri 60". Unawezaje kuendesha Serikali endelevu, thabiti na sikivu katika mazingira hayo ya kupanga na kupangua kila kukicha? Hakika kuwajibika na kuwajibishana ni muhimu katika kujenga utawala wa kitaasisi unaodumu kuliko utawala kinyonga na tegemezi kwa kiongozi mmoja mmoja.