Quantcast
Channel: UDADISI
Viewing all articles
Browse latest Browse all 468

Kwa nini Kusimamisha Majaribio ya GMO ni Ushindi?

$
0
0
Kwa Nini Uamuzi wa Serikali kusimamisha Majaribio ya GMO ni Ushindi kwa Tanzania?


Awali ya yote, nipende kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa usikivu wake na kuchukua hatua stahiki kuhusiana na sakata la mimea na mbegu Zilizobadilishwa Vinasaba (GMO) nchini. Kama mtafiti wa Uhuru wa Chakula, napenda kuihakikishia Serikali kuwa, wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, walaji, wazalishaji wa mbegu wa ndani, watafiti katika taasisi zetu za Kilimo (mbali na wale waliokuwa wakinufaika na mradi wa WEMA), na wauzaji wa vyakula nje na ndani ya nchi wamefarijika sana na hatua hii. Namshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, lakini pia natambua suala hili ni la kisera hivyo kwa namna yeyote linamhusu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania-Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Natoa pongezi za dhati kabisa kwa Serikali, na katika makala hii fupi nitaeleza kwa nini uamuzi huu ni wa kupongezwa.  

Kwanza, nianze kwa kukiri kuwa, hatua hii ambayo Serikali imechukua isingekwepeka katika nchi makini kama Tanzania. Lilikuwa ni suala la muda tu. Kuna watu wanaodhani maamuzi haya yamefikiwa kwa hofu tu isiyo na msingi wa kitafiti. Lakini nataka kuwatahadharisha kuwa Serikali ina taarifa nyingi zaidi kuliko sisi tunavyofikiri. Na kwa mwenendo wa kisera wa Serikali ya Awamu ya Tano, suala hili halikuhitaji mjadala wala barua za watu wasio na ushawishi wowote kutoka Mbinga au London. Lakini nitambue tu tamko la wakulima wenyewe, wakiwakilishwa na MVIWATA, huenda liliharakisha maamuzi haya muhimu kwa masilahi ya Taifa.  

Suala la kuruhusu teknolojia ya uhandisi-jeni, ni la kimkakati. Mara nyingi sana nimemsikia Rais akisisitiza Serikali inatekeleza Ilani ya CCM. Napenda kukumbusha tu kuwa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 ndiyo mkataba halisi kati ya Serikali na Wananchi waliokichagua chama hiki ili kitawale kuanzia mwaka 2015-2020. Tathmini ya kina inaonesha kuwa CCM haikuahidi teknolojia ya Uhandisi-jeni (Genetic Engineering) katika kilimo kupitia ilani yake ya mwaka 2015. Mkakati huu ungekuwepo kwenye Ilani huenda tungesema kuwa watu wameuchagua pale walipoipigia kura CCM. Kinachoshangaza ni pale ambapo katika Mpango wa Pili wa Sekta ya Kilimo (ASDP II), uhandisi-jeni katika mimea, wanyama na samaki unatamkwa kama mkakati ya Serikali katika kilimo. Hali hii inachanganya. 

Lakini pia tathmini ya kina inaonesha kuwa, mkakati ya uhandisi-jeni umekuwa ukisukumwa na makampuni husika yatakayonufaika na teknolojia hii kwa kuzitumia taasisi zetu za utafiti. Kimsingi, Sera ya Taifa ya Baiteknolojia (National Biotechnology Policy), iliyopitishwa mwaka 2010 ina kila harufu ya ushawishi wa hiki tunachokiona leo huku masilahi ya taifa yakiwekwa rehani. Kiutawala, taasisi za utafiti nchini si watunga sera bali watekelezaji wa sera na mikakati ya serikali iliyopo madarakani. Jukumu lao kuu ni kutoa utaalamu wa kitafiti kwa serikali ili kuiwezesha kutumia ushauri huo katika kutunga sera na mikakati husika. 

Katika sakata la mbegu za GMO, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) wamefanya tofauti. Naam, hawakutimiza wajibu wao. Taasisi hizi zimenukuliwa katika vyombo vya habari kama makuwadi wa kunadi mbegu za GMO kuwa zinakuja ili kumkomboa mkulima mdogo. Sera ya Baiteknolojia inatamka wazi katika kipengele cha malengo ya jumla kuwa inakusudia tu kutumia faida zilizothibitika za baioteknolojia, huku ikilinda usalama wa jamii na mazingira katika matumizi ya faida hizi. Hii inatuonesha kuwa, tayari waandaaji ya sera hii, pamoja na ubovu wake, walijua kuna madhara ya teknolojia hii.

Ukisoma Eneo la Sera (Policy Issue) 4.5, sera inataka umma wa Watanzania upate taarifa sahihi kuhusu teknolojia hii ili kuwasiadia wananchi na watunga sera kufanya uamuzi utakanao na ufahamu (informed decision) juu ya matumizi ya teknolojia hii kwa maendeleo. Kipengele hiki kinaendelea kusisitiza taasisi hizi kutoa taarifa sahihi na zenye mlingano wa faida na madhara ya teknolojia hii. Haiishii hapo tu, taasisi hizi zinahimizwa kuandaa midahalo na mijadala kuhusu faida na madhara ya matumizi ya teknolojia kwa afya, mazingira, uchumi na kimaadili. 

Lakini TARI na COSTECH waliamua kuchagua upande wa kuzungumzia faida tu za GMO kwa niaba ya wawekezaji wakati  tafiti lukuki za kisayansi zilizofanywa sehemu mbalimbali duniani zinasema kuna madhara, kama nilivyoeleza katika Barua yangu ya Wazi kwa Rais hapo awali. Tumefanya mijadala na wawakilishi wa taasisi hizi mara kadhaa, siyo walioandaa wao, ila walioalikwa lakini wamekuwa wakiimba faida za GMO tu bila kueleza ukweli kuhusu madhara. Mbali na kuwa hawakutoa elimu yenye mlingano wa faida na hasara, lakini pale ambapo watu walijitolea kutoa elimu hiyo, taasisi hizi zilitoa matamko ya kutaka kuzuia mjadala. Hali ilikuwa mbaya zaidi pale ambapo hata vyombo vya habari vilikuwa na upande wa kuzuia mawazo mbadala dhidi ya GMO.

Kimsingi, taasisi hizi zinazoendeshwa kwa kodi ya Watanzania hazikupaswa kutuchagulia teknolojia na kutumia wakulima kushawishi mbegu za GMO na teknolojia ya uhandisi-jeni zipitishwe chinichini kama mkakati wa nchi. Hazikupaswa kuendesha propaganda za kushawishi umma kuzipokea mbegu hizi bila taarifa sahihi juu ya faida na madhara. Kwa kuzingatia athari za kiuchumi zitokanazo na mbegu za GMO, COSTECH na hasa TARI walipaswa kuhimiza utafiti unaoendana na kilimo chetu na kuwa mhimili mkubwa wa mageuzi ya kilimo nchini. Kiujumla, taasisi hizi hazikupaswa kuwa makuwadi wa makampuni ya nje yanayokusudia kutuletea ukoloni wa kikampuni. 

Kwa upande wa serikali yetu tukufu, kuruhusu kuanza kwa utafiti, na baadaye kutoa rukhsa ya matumizi ya mbegu za GMO ni jambo ambalo yafaa umakini uzingatiwe. Nafurahi kuona kuwa kanuni zetu za usalama wa viini hai (biosafety), zinaweka tahadhari kubwa sana, japo pamekuwa na jitihada za kuzimwagia maji kwanza kuruhusu utafiti. Lakini kuruhusu matumizi ya mbegu za GMO zenye athari katika maisha ya makundi mbalimbali niliyoyataja hapo juu, na nafasi yetu ya kuuza chakula ndani na nje ya nchi, ni suala ambalo haliwezi kuchukuliwa kwa wepesi. Kwa namna yeyote serikali ilipaswa kupata ridhaa ya jamii za asili za maeneo hayo (indigenous peoples) hasa kwa kuzingatia fasili ambayo inahusisha wakulima wadogo kwa misingi ya kanuni ya Free, Prior and Informed Consent(FPIC), yaani uhuru wa kuridhia kabla ya kitu fulani kufanyika.

Kanuni hii ya ridhaa ya jamii husika inawekwa na mikataba ya kimataifa kama vile Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Jamii za Asili (UNDRIP), Mkataba wa Shirika la Kazi namba 169 (ILO Convention 169), na Sera kuhusu Jamii za Asili na Watu wa Makabila iliyoandaliwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO). Sheria za kimataifa zinaweka wazi haki ya kujitawala (Right to self-determination) kwa jamii hizi ambayo ndiyo msingi mkubwa wa kuhakikisha kuna ridhaa kutoka kwa jamii za asili zinazoishi na kutegemea maeneo yanayolengwa. Hivyo basi, jambo linalobadili maisha yao kama hili la mbegu za GMO, kiuchumi, kimazingira na hata kiafya lilipaswa kupata ridhaa ya wakulima wadogo, ambao kimsingi ni asilimia kubwa ya wananchi wetu. Ukiniuliza mimi, kwa kuwa GMO inagusa pia jamii kubwa ya walaji wa mijini na vijijini, uamuzi huu unahitaji kura ya maoni (referendum).  

Lakini kuna baadhi ya watu wanaona ni jambo la ukakasi kuzuia utafiti huo wa GMO. Hoja hii imepata mashiko makubwa na inaoneka kuzuia utafiti ni kutokupenda  sayansi. Ieleweke pia, kupinga GMO inaonekana pia kama ni kupinga sayansi. Wasiwasi mkubwa pia umeoneshwa na baadhi ya wanafunzi wanaotaka kubobea katika teknolojia hii, wakihofu kuwa sasa hawatapata fursa ya kufanyia kazi ujuzi wao. 

Lakini utafiti wa GMO uliofanyika Makutupora-Dodoma ulikuwa na mwelekeo upi? Mwelekeo wa tafiti hizi ulikuwa kuhalalisha tu mradi wa mbegu za GMO kwa kuzitumia taasisi zetu. Utafiti huu haukuwa HURU wenye lengo la kuleta matokeo mapya, kama vile kujibu ukosoaji wa kisayansi uliofanywa na tafiti za wanasayansi wengine waliogundua athari mbalimbali za GMO katika mazingira, baianuai, na mtanzuko wa kisayansi juu ya usalama wa vyakula vya GMO kiafya. Inaonekana utafiti huu ulilenga uzalishaji tu kisha watafiti wanaumbaumba ripoti za tathmini za kiuchumi na kimazingira ili kuurubuni umma kuwa GMO hazina madhara yeyote. Na kimsingi, utafiti huu ulifanywa katika mazingira magumu ya hakimiliki (patent) ambapo wanasayansi wetu hawakuwa na uwezo wa kuifikia teknolojia halisi ya uhandisi-jeni bali kufanya majaribio ya kukuza mimea tu katika eneo la majaribio. Kampuni ya Monsanto imekuwa ikifanya majaribio ya aina hii katika kila nchi kama hatua ya kulazimisha mbegu na vyakula vya GMO vikubalike huku yenyewe ikiwa inahakikisha inahodhi hakimiliki mbalimbali za mbegu.

Ikumbukwe kuwa, Afrika Kusini, ambao walirasimisha matumizi ya GMO nchini mwao tangu miaka ya 1990 wiki iliyopita walikataa kuidhinisha mbegu za mahindi za Monsanto MON87460, MON89034, na NK603 zilizotajwa kuhimili ukame na wadudu. Lakini tathmini binafsi zilionesha kuwa uwezo wa mbegu hizi haukutofautiana na mbegu zinazozalishwa kawaida, na katika majaribio mengine mbegu za GMO zilikuwa na mazao hafifu kuliko mbegu za kawaida. Hii inadhihirisha kwamba Afrika Kusini wameanza kung’amua ujanja wa makampuni haya wenye lengo tu la kulikamata soko la mbegu. Lakini pia utafiti huu wa Afrika Kusini ulichukua miaka takribani mitano, lakini utashangazwa na utafiti wa miaka miwili (2016-2018) wa Makutupora halafu wanasema wakulima wanazihitaji hizo mbegu haraka, hata kabla tathmini huru haijafanyika. Utafiti huu haukuwa na malengo sahihi kwa masilahi ya Taifa na serikali ilikuwa na kila sababu ya kuupiga tindo.

Tathmini iliyofanywa na Chuo Cha Ulinzi cha Marekani mwaka 2011, inaeleza kuwa kuna uwezekano wa maadui kutumia GMO kama silaha ya kibaiolojia na kuleta madhara makubwa sana kwa jamii. Ripoti hii ya utafiti inatufungua macho kujua ni kwa jinsi gani teknolojia hii inapaswa kuchukuliwa kwa umakini. Mimi naunga mkono utafiti. Lakini kwanza ningeshauri Serikali iwekeze katika teknolojia hii na kupata wataalamu watakaoweza kufanya uhandisi-jeni wenyewe. Na taasisi zetu za kiusalama zinaweza kuwa mwangalizi mzuri wa tafiti hizi zenye lengo la kujielimisha kwa kushirikisha taasisi zingine na watafiti binafsi nchini. Hatuwezi kuacha uwekezaji huu kwa makampuni ya nje bila serikali kujiridhisha kuhusu faida na madhara ya teknolojia hii. Ningetamani watafiti wa Tanzania waje na matokeo huru ya faida na hasara za GMO. 

Lakini pia si lazima tufanye utafiti wa kila kitu hasa kama tuna vipaumbele vingine. Tafiti inapaswa kuwa kwa ajili ya msaada wa nchi, na teknolojia ni chombo cha kuleta maendeleo lakini si dira ya maendeleo. Tathmini inaonesha kuwa teknolojia ya uhandisi-jeni ni ghali, ila hatuwezi kusema tunachelewa kupata teknolojia hii. Ningeshauri tafiti zetu zijikite zaidi katika maeneo mengine ya kilimo ili kuboresha mbegu zetu zinazoweza kuzaa kawaida, kwani tafiti zinaonesha kuna uwezekano wa kuwa na mbegu za kawaida zinazohimili ukame na kuleta tija kubwa. Ni jambo la kushangaza pia kuwa Monsanto wana mbegu za kawaida zinazohimili ukame lakini wanaona hazitawapa mamlaka ya kutosha juu yetu.

Ujasiri wa Serikali ya Awamu ya Tano kuzuia majaribio ya GMO unatutia moyo sana. Pamoja na mambo mengine, Serikali ya CCM ikiongozwa na Rais Magufuli imekuwa jasiri katika kufufua ATCL kwa kununua ndege mpya; ujenzi wa reli (Standard Gauge Railway-SGR) ili kuboresha miundombinu na sekta ya usafirishaji; kuhakikisha taifa linanufaika na rasilimali zake kama vile madini katika sakata maarufu la makinikia; na imesimama thabiti katika nia ya kujenga bwawa la kuzalisha umeme (Stiegler’s Gorge Hydropower Plant), hatua ambayo itatupatia umeme wa uhakika. Katika mkakati wa viwanda, tumebakiza mkakati thabiti tu wa kuhakikisha Mkulima Mdogo analipeleka jembe la mkono Makumbusho ya Taifa, kwa kujengwa viwanda vinavyotengeneza zana za bei nafuu na za kisasa (motorized simple and affordable farm implements) zitakazoongeza tija katika uzalishaji.
 Pia tunahitaji utekelezaji wa Azimio la asilimia 1 ya pato la taifa kuelekezwa katika tafiti, ili taasisi zetu za kilimo ziweze kujikita katika kuboresha mbegu zinazoendana na utamaduni wa chakula chetu. Na mwisho Serikali inapaswa kuhakikisha mkulima ananufaika na kilimo kwa kuweka mazingira wezeshi ya soko la uhakika la ndani na kufungua mipaka ya nje ili Tanzania iwe inauza chakula bora na kisicho na unyanyapaa katika ukanda wa SADC, na Afrika Mashariki. Ukisoma Ilani ya CCM 2015 ukurasa wa 14-16 haya, na mambo mengine, ndiyo wakulima waliyategemea katika ASDP II na utekelezwaji wake mpaka 2020. 

Katika kufanikisha hayo, tunahitaji mikakati sahihi na GMO, mbegu na chakula chenye unyanyapaa duniani, haiwezi kuwa sehemu ya mkakati huo. Niliwahi kusema huko nyuma, Tanzania kama kitovu cha utalii Afrika tunapaswa kulinda vyakula vyetu kwa choyo kubwa, ili tusiwakwaze watalii wetu. Lakini pia kwa kuzingatia uwezo wetu wa kuzalisha, ambao mpaka sasa hatujauendeleza vya kutosha, ningetamani kuona Tanzania inakuwa chanzo cha uzalishaji na usambazaji wa vyakula salama Afrika huku vikiwanufaisha wakulima wetu na kuchangia ukuaji wa pato la Taifa na maendeleo.

Naipongeza tena Serikali kwa uthubutu na kuchukua maamuzi sahihi bila kupepesa macho. Katika sakata hili la kuzuia GMO nchini, Watanzania wameshinda. Pasi na shaka, uamuzi huu utakumbukwa siku za usoni.

Mungu Ibariki Tanzania!

Viewing all articles
Browse latest Browse all 468

Trending Articles